We have been officially sponsored by:

Saturday, 20 April 2013

Terry achafua hali ya hewa tena!

Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya England, John Terry amechafua hali ya hewa kwa kukataa mkono wa bosi wa FA. Terry ambaye pia ni nahodha wa Chelsea, alikataa mkono wa Mwenyekiti wa FA, David Bernstein wakati wa hafla ya kurudisha kombe la Ubingwa wa Ulaya. Terry alikiri kwa macho makavu kwamba alikataa kupokea mkono wa Bernstein, lakini mwenyekiti huyo alidai hakumaizi hilo, ila akasema ni upuuzi mtupu. Hilo lilikuwa tukio kubwa kimataifa kwa soka, kwani wakuu wa Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) walikuwapo, akiwamo bosi wao, Michel Platini, ambapo timu yenye kombe hulikabidhi. Chelsea walitwaa kombe hilo mwaka jana, na wakavunja rekodi vibaya kwa kuwa timu ya kwanza kushindwa kuvuka hatua ya makundi katika mashindano yaliyofuata. Mbaya zaidi ni kwamba fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka huu zinafanyika katika Uwanja wa Wembley. Timu nne zilizofuzu hatua ya nusu fainali ni Barcelona, Bayern Munich, Borussia Dortmund na Real Madrid, jozi za kwanza zikichuana kama ilivyo kwa jozi za pili. Terry atakuwa amekasirishwa na uamuzi wa mwisho wa Bernstein wa kumvua unahodha wa England baada ya mchezaji huyo kuwa ameshitakiwa kwa kumkashifu kibaguzi mweusi Antony Ferdinand wa QPR. Uamuzi huo ulisababisha aliyekuwa kocha wa England, Fabio Capello kujiuzulu, ambapo licha ya mahakama kumsafisha Terry katika hoja zilizozidisha utata, FA ilimtia hatiani na kumpa adhabu. Terry alifungiwa mechi nne na £220,000, jambo lililomchukiza na kuamua kuachana na timu ya taifa. Hata hivyo wadau wengi walichukulia kwamba adhabu hiyo haikuwa kubwa vya kutosha. Alipoulizwa Ijumaa kwa nini hakupokea mkono wa mwenyekiti, Terry alisema: “Sikiliza, hili ni jambo gumu kwangu. Ni wazi ndiye aliyesimama kunikandamiza kwenye ile kesi mahakamani, akasema vitu nisivyotaka kusema hewani, nadhani ni suala tunalotakiwa kuepuka tu.” Mwenyekiti wa FA, Bernstein ambaye amebakisha miezi michache aondoke madarakani, alisema haya kuhusu suala lake na Terry hiyo jana: “Sikumaizi chochote, uhusiano wangu na kila mmoja hapa ni mzuri…nadhani tuzungumzie mambo chanya zaidi kuliko upuuzi. Alipobanwa kuhusu uhusiano wake na Terry, Bernstein alisema wapo mbali mbali kidogo, lakini akasema si jambo linalomfikirisha, kwa sababu ana mengi ya vipaumbele kufanyia kazi kwa muda wake mfupi uliobaki.

Sunday, 24 March 2013

Tanzania yatikisa Kombe la Dunia (Kufuzu)

*Kenya waibana Nigeria, Ivory Coast wapaa *Bafana, Burkinafaso, Ethiopia nao wachanja *Cameroon, Malawi, Ghana safi, Zambia mh... Taifa Stars wameipandisha chati Tanzania, kwa kuwa gumzo baada ya kuwafunga Morocco kwenye mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2014. Wakicheza nyumbani mbele ya maelfu ya washabiki wao, Stars waliwaaibisha Simba wa Milima ya Atlas kwa kuwakandika mabao 3-1. Morocco wanapigania kufuzu kucheza kombe hilo mwakani nchini Brazil kwa mara ya kwanza tangu 1998, lakini ndoto zao zilitibuliwa na wanandinga wanaopiga soka ya kulipwa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. AlikuwaThomas Ulimwengu aliyefunga bao la kwanza muda mfupi kabla ya mapumziko, kisha Mbwana Samatta wa TP Mazembe pia akafunga mabao mawili dakika ya 67 na 80 ya mchezo uliopigwa Dar es Salaam. Morocco hawakuamini matokeo hayo, kwani yamefifisha ndoto zao kurejea kilinge cha dunia, ambapo mshambuliaji wao anayekipiga Granada ya Hispania, Youssef El-Arabi alifunga bao la kufutia machozi dakika za majeruhi. Kwa ushindi huo, Tanzania wanapanda hadi nafasi ya pili ya kundi ‘C’ wakiwa na pointi sita, wakati Morocco ni wa tatu kwa pointi zao mbili, huku wakibakisha mechi tatu. Ivory Coast ndio wanaoongoza kundi hilo, na hawakujutia kumtosa nahodha wao, Didier Drogba, kwani walipata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Gambia. Kocha Sabri Lamouchi wa Ivory Coast alitamba kwa kikosi chake, ambapo mabao yalifungwa na Wilfried Bony, Yaya Toure na Salomon Kalou. Ivory Coast wanaongoza kundi lao la ‘C’ kwa pointi nne, na wanakaribia kabisa moja ya nafasi tano zilizotengwa kwa ajili ya bara la Afrika nchini Brazil mwakani. Mabingwa wa Afrika, Nigeria wameambulia pointi moja baada ya kutoka sare na Kenya. Hii ilikuwa mechi ya kwanza ya Nigeria tangu walipotwaa ubingwa kwa kuwafunga Burkina Faso, ambapo hadi dakika ya 93 walishalala kwa bao moja lililofungwa na Francis Kahata, katika mtiti uliopigwa Calabar. Hata hivyo, alikuwa Nnamdi Oduamadi aliyetokea benchi na kuwafundisha jinsi ya kufunga nyota wengine wa kimataifa ambao hawakung’ara dimbani, Obafemi Martins, Sunday Mba na Victor Moses. Kwa sare hiyo, Nigeria wamewaacha Malawi waungane nao kuongoza kundi lao, kwani waliwashinda Namibia kwenye mechi nyingine wikiendi hii. Katika mechi ya Malawi dhidi ya Namibia, Frank Mhango ndiye aliwapatia Wanyasa bao pekee, huku wakiwa bila kocha wao wa muda, aliyelazimika kwenda kumzika mwanawe aliyefariki dunia kwa saratani. Namibia wana pointi tatu kutokana na mechi tatu kwenye kundi lao la ‘F’ na Kenya wanashika mkia wakiwa na pointi mbili tu. Nyota mwingine wa soka ya Afrika, Samuel Eto'o alirejea kuwatumikia Cameroon, akafunga mabao mawili walipowashinda Togo 2-1. Ushindi huo unatoa mwanya kiasi fulani kwa Cameroon kufuzu kushiriki mashindano makubwa kwa mara ya kwanza tangu 2010. Dove Wome alisawazisha moja ya mabao ya Eto’o, lakini nyota huyo alirejesha tofauti ya bao. Togo haikuwa na nyota wake, Emmanuel Adebayor, golikipa Kossi Agassa na wengine kadhaa wanaoendesha uasi dhidi ya kocha wao, Didier Six, timu yao ikishika mkia kwa pointi moja. Afrika Kusini waliokuwa wenyeji wa mwisho wa Kombe la Dunia, wamerejesha matumaini ya kushiriki mwakani, baada ya kuwafunga Jamhuri ya Afrika ya Kati 2-0 jijini Cape Town, kwa mabao ya Thabo Matlaba na Bernard Parker. Bafana waliongoza kundi ‘A’ kwa muda kabla ya Ethiopia kuwaondosha hapo Jumapili hii. Wahabeshi wameonesha dhamira ya kurejea kwenye soka ya kimataifa, baada ya kuwakung’uta Botswana 1-0, wakafikisha pointi saba na kushika usukani wa kundi hilo kwa tofauti ya mbili. Tunisia walijihakikishia udhibiti wa kundi ‘B’ baada ya kuwafunga wanaoshika nafasi ya pili, Sierra Leone kwa mabao 2-1 mjini Rades. Burkina Faso waliomaliza nafasi ya pili katika Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka huu, waliwananga Niger 4-0 katika mtiti wa kundi ‘E’ uliopigwa jijini Ouagadougou. Vinara wa kundi hilo, Congo Brazzaville walifikisha ushindi wa tatu katika mechi tatu, baada ya kuwabandua Gabon 1-0 jijini. Beki wa Queen Park Rangers (QPR), Christopher Samba ndiye alifunga bao hilo, akitafuta sasa kucheza Kombe la Dunia mwakani, hata kama QPR inayoshika mkia Ligi Kuu ya England (EPL) itashuka daraja. Senegal walitoka sare na Angola, hivyo kuwaweka pointi mbili mbele ya Waangola hao katika kundi ‘J’ jijini Conakry, mechi ilikochezwa kwa vile uwanja wa Leopold Senghor wa Dakar, Senegal umefungiwa kwa mwaka mmoja kutokana na fujo za mwaka jana. Senegal wanaongoza kundi lao kwa pointi tano. Lesotho waliwashangaza mabingwa wa zamani wa Afrika, Zambia, kwa kutoshana nao nguvu dimbani. Zambia walicheza kipindi cha pili wakiwa 10, baada ya golikipa wao, Kennedy Mweene kulambwa kadi nyekundu. Walikuwa wakiongoza hadi dakika ya 89, Lesotho waliposawazisha. Kocha wa Zambia, Herve Renard ameonya kwamba wanaweza kujutia pointi mbili walizopoteza. Zambia, hata hivyo, wanaongoza kundi ‘D’ kwa tofauti ya pointi moja, baada ya matokeo ya Jumapili hii, ambapo Ghana waliwachapa Sudan 4-0. Kundi la washindi 10 kutoka makundi haya ya awali, litaingia kwenye raundi ya mwisho kwa kucheza mechi mbili, nyumbani na ugenini ili kupata watakaokwenda Brazil mwakani.

Thursday, 21 March 2013

Rais JM Kikwete, aufungua rasmi uwanja wa Azam FC

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Jakaya Mrisho Kikwete hii leo amezindua uwanja wa klabu ya Azam FC inayomilikiwa na makampuni ya Said Salim Bakhresa ya jijini Dar es Salam. Rais Kikwete amezindua rasmi uwanja huo wa unaojulikana kwa jina la Azam Complex uliopo nje kidogo ya mji wa Dar es salam eneo la Mbande,huko Mbagala wilayani Temeke. Azam ilianza kuutumia uwanja huo mapema mwaka 2011 mara baada ya kupata cheti cha FIFA chenye namba za usajili AF3243.1,ambacho kilithibitisha matumizi wa kiwanja hicho chenye nyasi bandia kutumika mpaka mwezi wa tatu mwaka 2015. Uwanja huo umekuwa ukitumika kwa michezo mbalimbali ya ligi kuu soka Tanzania bara na pia michuano ya kombe la Kagame linaloshirikisha klabu bingwa Afrika Mashariki na kati pamoja na Michuano ya kombe la CECAFA Senior Challenge ambalo hushirikisha mataifa ya ukanda wa Afrika mashariki na Kati. Klabu ya Azamu ambayo imekuwa na mafanikio makubwa kwa miaka ya karibuni toka ipande daraja la ligi kuu soka nchini Tanzania misimu minne iliyopita ambapo mwaka huu kwa mara ya kwanza wamefanikiwa kushiriki michuano ya kimataifa ya kombe la shirikisho barani Afrika baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu Tanzania bara msimu uliopita nyuma ya Simba. Klabu hiyo inayonolewa na kocha Muingereza Stewart Jan Hall,Inakuwa klabu ya kwanza nchini Tanzania kumiliki uwanja wake wa kisasa ambao unawezesha zaidi ya mashabiki elfu 30 kukaa jukwaani kutama mpira. Kwenye uwanja huo,Azam pia ina hosteli au mabwalo ya kukaa wachezaji ambapo wamejenga kituo maalumu cha kuendeleza timu zao za vijana maarufu kama Academy. Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya Said Salim Bakhresa,Bwana Aboubakari Bakhresa ameiambia Tanzania Sports kuwa,wanajivunia mafanikio ambayo wamekuwa nayo kwa siku za karibuni. Azam Imekuwa na mchango mkubwa katika timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars ambayo wikiendi hii itakuwa uwanjani kucheza na Morocco katika mchezo wa kusaka tiketi ya kushiriki kombe la dunia hapo mwakani,ambapo kwenye kikosi cha Kim Poulsen kocha wa timu ya taifa ya Tanzania,Azam ina wachezaji sita kati ya 23 walioitwa kuunda timu hiyo. Azam inatarajia kucheza mechi yao ya kimataifa majuma mawili yajayo nyumbani,watakapo wavaa BYC ya Liberia katika mchezo wa marudiano wa kombe la shirikisho raundi ya pili ambapo katika mchezo wa kwanza Azam iliichapa timu hiyo kwa mawili kwa moja. Link ya uwanja wa Azam kuwa miongoni mwa viwanja vilivyothibitishwa na FIFA kwa Ubora wake. http://www.fifa.com/aboutfifa/organisation/marketing/qualityprogramme/footballturf/producers/producer=15.html

Tuesday, 12 March 2013

LIGI YA VODACOM KUENDELEA J’MOSI

Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea Jumamosi (Machi 16, 2013) kwa mechi tatu zitakazochezwa katika miji ya Mwanza, Dar es Salaam na Manungu, Turiani mkoani Morogoro. Toto Africans inayopigana kukwepa kurudi daraja la kwanza itakuwa mwenyeji wa Mgambo Shooting kutoka Tanga katika mechi itakayochezwa Uwanja wa CCM Kirumba. Vinara wa ligi hiyo Yanga wataumana na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa wakati Uwanja wa Manungu utakuwa mwenyeji wa mechi ya Mtibwa Sugar na Coastal Union. UCHAGUZI TAFCA KUFANYIKA MOROGORO Uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) utafanyika Jumamosi (Machi 16 mwaka huu) mjini Dodoma ambapo wajumbe wanatakiwa kuripoti siku moja kabla ya uchaguzi. Wagombea waliopitishwa kuwania uongozi na Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA chini ya uenyekiti wa Ramadhan Mambosasa ni Oscar Don Koroso (Mwenyekiti), Lister Manyara (Makamu Mwenyekiti) na Katibu (Michael Bundala). Wengine ni Gabriel Gunda (Katibu Msaidizi), Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania- TFF (Wilfred Kidao) wakati wagombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni Jemedali Saidi, George Komba na Magoma Rugora. KIM KUTAJA KIKOSI CHA KUIKABILI MOROCCO Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Kim Poulsen anatarajia kesho (Machi 13 mwaka huu) kutaja kikosi chake kitakachoivaa Morocco. Mkutano huo wa Waandishi wa Habari utafanyika saa 5 asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itacheza na Morocco kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Machi 24 mwaka huu. MECHI YA SIMBA, COASTAL YAINGIZA MIL 37/- Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Coastal Union iliyochezwa juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 36,820,000 kutoka na watazamaji 6,284. Viingilio katika mechi hiyo namba 138 iliyomalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 8,265,752.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 5,616,610.17. Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 4,202,924.97, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 2,521,754.98, Kamati ya Ligi sh. 2,521,754.98, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 1,260,877.49 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 980,682.49.

Sunday, 10 March 2013

FIFA Isipewe kila kitu katika Nchi Zetu....

UKIINGILIA masuala ya soka per se, unatafuta vita na Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA) hata kama wewe ni nani katika nchi yako uliye nje ya uongozi wa soka wa nchi. Zaidi, wewe ukiwa serikali ndiyo kabisa hutakiwi kuingilia soka ya nchi yako, lakini unaweza kumlipa kocha wa taifa, kulipia kambi ya timu ya taifa, kusafirisha timu ya taifa kwenda nje ya nchi kushiriki mashindano na kadhalika. Maamuzi ya watu wa soka kwa soka yao usiyaguse hata wakifanya maamuzi ya ajabu na ya ujinga uliopitiliza! Hivi ndivyo unavyoweza kuyaeleza kwa ufupi "maagizo" makali ya FIFA kulinda soka yao duniani dhidi ya dola za nchi. Kimsingi, soka sasa inaonekana kuwa ni mhimili unaojitegemea wa nchi, kwani hata ikijadiliwa bungeni maazimio ya Bunge ili yatekelezwe, lazima utekelezaji huo ufanywe na Serikali au Mahakama wakati Serikali haitakiwi kuingilia masuala ya soka, huku masuala hayo yakiwa hayapaswi kufikishwa wala kuamuliwa mahakamani. Kwa msingi huo, mihimili yote ya dola imefungwa mikono kuweka sawa masuala ya soka yanapovurundwa na kufumbiwa macho na watu wa soka wenyewe au uvurundaji huo unapofanywa kwa maslahi ya wenye sauti miongoni mwa watu wa soka. Katika utaratibu wa mgawanyo wa mamlaka (separation of power) miongoni mwa Serikali (executive), Bunge (legislature) na Mahakama (judiciary), kuna utaratibu wa kudhibitiana (check and balance) ili mhimili mmoja usitumie mamlaka yake ovyo ovyo kwa kujiona hauna wa kuhoji utendaji wake. Bunge linajadili na kutoa maazimio dhidi ya serikali na mahakama zinapotenda kinyume, ambapo kwa mahakama si kwa jinsi zilivyoamua kesi. Mahakama zinatafsiri sheria za Bunge na kutengeneza misingi mipya ya kisheria katika kutafsiri huko na zinaamua kesi za utawala dhidi ya serikali kwa kuweka misingi mizuri ya kisheria ya utawala bora. Serikali nayo ina mchango katika uongozi wa Bunge kwa kupitia kwa kiongozi wake bungeni ambaye ni waziri mkuu. Aidha, Serikali yenyewe ndiyo hupeleka miswada bungeni ya kupitishwa kuwa sheria. Kwa upande mwingine, Serikali ni mteuzi wa majaji ili kuhakikisha mhimili wa Mahakama unakuwa na watenda haki walio bora. Kwa bahati mbaya kwa soka, hakuna udhibiti huo toka mhimili wowote wa dola baada ya zuio la FIFA kwamba soka isiingiliwe. Kimsingi, ni sahihi sana kuzuia soka isiingiliwe kwani hali hiyo ingeruhusiwa, mambo mengi ya soka yangechelewa kwani kila mara, kila chombo kingekuwa kinakuja na maelekezo yake ya nini kifanyike lini na hata mahakama zingetumika kusimamisha mashindano kwa amri ya muda (injunction) mpaka uamuzi fulani utolewe. Hapo hata kalenda za soka zingekuwa matatizoni. Lakini sasa kinachokera ni kwa maelekezo hayo ya FIFA kutumika Tanzania kana kwamba FIFA hiyo sasa ni rais wetu namba moja anayesaidiwa na namba mbili wake, Jakaya Mrisho Kikwete katika masuala yoyote yanayogusa utawala wa soka hata kama si ya soka per se! Mfano wa hivi karibuni ni wa suala la serikali kupinga utaratibu wa uandikwaji wa katiba mpya ya TFF. Hili ni suala la kukumbushana kufuata sheria za nchi na si suala la soka. Kama katiba iliyopo inatengeneza hali ya ulazima (mandatory) wa katiba mpya kutengenezwa na mkutano mkuu, ikitengenezwa kwa kuipitisha kwa wajumbe wa mkutano mkuu kuisoma na kuamua (secular resolution) inakuwa imetengenezwa kinyume cha katiba isipokuwa tu katiba hiyo ikiwa kimya kwa hilo. Hata kwa tafsiri ya maneno kwenye katiba, ‘mkutano mkuu’ kwa tafsiri ya kisheria ni tofauti na ‘wajumbe wa mkutano mkuu’. Mkutano Mkuu ni mkusanyiko wa mahali fulani na wajumbe wa mkutano mkuu ni watu wanaoweza kuwa pamoja au walio sehemu mbalimbali. Katiba ikisema katiba itapitishwa na mkutano mkuu, lazima ipitishwe na mkusanyiko mmoja wa wajumbe, lakini ikisema itapitishwa na wajumbe wa mkutano mkuu inaweza kuwa kwa mkusanyiko au kwa kuipitisha kwao waitolee maoni kwa kuwaendea kokote waliko bila kuwepo mkusanyiko. Serikali, kupitia mamlaka zake za usajili wa katiba za vyama vya michezo, inaiona katiba ya chama cha mchezo wa soka imepitishwa kwa ukiukwaji, inaelekeza ipitishwe kwa taratibu sahihi. Hapo soka imeingiliwaje na serikali? Nani atarekebisha kosa la TFF la ukiukwaji wa uandishi wa katiba yao? TFF wenyewe wanaoamini hawakukiuka chochote? Lazima kuwe na ‘check and balance’ jamani. Tusifikie mahali pa kuipa FIFA uwezo wa kuwa kama rais wetu katika masuala yanayohusu watu wa soka. Leo serikali inashughulikia utaratibu wa utengenezaji wa katiba ya chama cha soka (siyo yaliyomo kwenye katiba), madai yanatolewa kwamba serikali imeingilia soka. Kesho mtu wa soka ataiba fedha za chama cha soka, mtasema asichuliwe hatua na vyombo vya serikali kwa sababu FIFA imezuia serikali kuingilia mambo ya soka na mwisho mtu wa soka akimuua mwenzake kwenye mkutano wa chama cha soka mtasema hilo ni suala la soka. Hebu tuweke mpaka wa mambo ya soka na yasiyo ya soka katika kushughulikia mambo yetu ya ndani ya nchi, ili tusiipe FIFA urais wa nchi yetu katika masuala ya soka. Serikali ya Tanzania ipo sahihi kuhakikisha TFF inapata katiba kwa njia sahihi. Maagizo hayo yapo mbali na soka kwani hayagusi vipengele vya katiba hiyo.

Thursday, 7 March 2013

Arsenal wamtaka Williams wa Swansea

*Watenga £ mil. 8 kumchukua beki Williams *Wapanga safari Vietnam kujiimarisha Julai Arsenal wameanza kuangalia ‘maisha baada ya msimu huu mbaya’, kwa kutaka kumsajili nahodha wa Swansea, Ashley Williams na kwenda Vietnam. Baada ya msimu unaowaendea vibaya ambapo si ajabu wakakosa nafasi kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya, Arsene Wenger sasa amekiri hana beki. Katika hilo, ametenga pauni milioni nane kwa ajili ya kumng’oa nahodha na mkoba wa Swansea, Ashley Williams. Ama kwa safari na mechi kabla ya msimu ujao, Arsenal wametenga siku tatu za kukaa Vietnam, na watakuwa timu ya kwanza ya Ligi Kuu England kwenda huko kwa ‘vichaa’ wa soka. Vietnam ina watu milioni 90 na ni taifa la wapenda soka, hivyo Arsenal wanaona ni eneo muhimu kuongeza mashabiki wake. Arsenal wanao pia mashabiki wengi kutoka bara la Afrika na Asia na wamekuwa na utamaduni wa kuwa na wachezaji mchanganyiko wa rangi kwenye kikosi chao. Wakiwa mji mkuu wa Vietnam, Hanoi, Arsenal wamepanga kuchezesha kikosi kamili dhidi ya timu ya taifa ya nchi hiyo ya kikomunisti kati ya Julai 15 na 17 kwenye Uwanja wa Taifa wa My Dinh. Kwa miaka kadhaa, Arsenal wamekuwa wakisaidia miradi ya soka ya Vietnam kwa ajili ya kukuza wachezaji chipukizi kupitia Hoang Anh Gia Lai-Arsenal JMG Academy. Tayari wametangaza mechi nyingine jijini Jakarta, Indonesia na nyingine katika nchi ambayo haijatajwa barani Asia. Imekuwa kawaida Arsenal kwenda Austria kabla ya msimu kuanza, lakini shinikizo za kibiashara zimewasukumia Asia miaka ya karibuni. Liverpool, Manchester United, Chelsea na Manchester City nao pia wanatarajiwa kukwea pia hadi Asia kwa ajili ya mechi za maandalizi ya msimu ujao. Baada ya ulinzi dhaifu mwishoni mwa wiki iliyopita dhidi ya Tottenham Hotspurs ambapo Arsenal walilala kwa mabao 2-1, imedhihirika wameanza kupoteza imani na walinzi wake wa kati, nahodha Thomas Vermaelen na Per Mertesacker. Mabao yote mawili ya Spurs yaliyofungwa na Gareth Bale na Aaron Lennon yalikuwa laini na yanayozuilika na wadau wameinyooshea kidole beki. Williams anakadiriwa kugharimu pauni milioni nane, lakini Arsenal wanaweza kulazimika kuongeza dau, kwani Brendan Rodgers wa Liverpool naye anamwangalia kijana huyo huyo mwenye umri wa miaka 28. Williams ni nahodha wa Timu ya Taifa ya Wales na Wenger anaamini ni mtu mwenye tunu za kiuongozi anayeweza kupanga na kudhibiti mfumo wa ulinzi wa Arsenal. Anataka kuurejesha ukuta huo enzi zile za mafanikio, ukiwa chini ya watu kama Tony Adams, Martin Keown au Steve Bould ambaye sasa ni kocha msaidizi wa Arsenal na mtaalamu wa kunoa mabeki. Williams ana mkataba hadi 2015, ndiyo maana gharama yake inatarajiwa kwenda hadi £8m. amekuwa nguzo ya mafanikio ya Swansea tangu alipojiunga akitoka Stockport County enzi za kocha Roberto Martínez. Kwa miaka mitano sasa amejijenga kwenye safu ya ulinzi, akiwa mahiri katika kuusoma mchezo na kutambua nguvu na udhaifu wa wapinzani upo wapi, kuwapanga wenzake na kuwajibika mwenyewe. Ukosefu wa mchezaji wa aina hiyo ndio umekuwa kiini cha Arsenal kupoteza mechi muhimu kama ya Spurs, kiasi cha kuachwa nafasi ya tano, wakiwa nyuma yao kwa pointi saba. Imebaki michezo 10 kwa kila timu ya ligi kuu England, na Arsenal wanajaribu kukwepa kumaliza nyuma ya Spurs, jambo ambalo halijatokea tangu 1995, Gerry Francis alipokuwa kocha White Hart Lane.

Monday, 25 February 2013

Hatimaye Serikali ya Tanzania yaingilia mgogoro wa TFF

SERIKALI imeliagiza Shirikisho la Mchezo wa Mpira wa Miguu nchini (TFF) kufuta matumizi ya Katiba ya Shirikisho hilo ya mwaka 2012 badala yake watumie Katiba ya mwaka 2006 kwa kuwa Katiba ya mwaka 2012 imekiuka kanuni za Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa ( BMT) Na.11 (1). Agizo hilo limetolewa leo na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe. Dkt. Fenella Mukangara alipokuwa akiongea na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam kuhusu mgogoro wa uchaguzi wa Viongozi wa TFF. Dkt. Mukangara pia ameiagiza TFF kufuata utaratibu wa kurekebisha Katiba za vyama vya michezo, kwa mujibu wa Sheria ya BMT iliyotungwa na Bunge pamoja na kanuni zake ambazo ziko wazi na rahisi kuzifuata. Alifafanua kuwa TFF walikiuka Sheria Na. 12 ya Baraza la Michezo la Taifa na marekebisho yake Na.6 ya mwaka 1971 pamoja na kanuni za usajili Na. 442 za mwaka 1999. “Kanuni ya BMT Na. 11(1) inaeleza wazi utaratibu wa marekebisho ya Katiba ambapo walitakiwa wajaze Fomu Na. 6,7,8 na 9 kisha baada ya siku 14 Msajili wa vyama vya michezo anatakiwa kuwajibu, kama anakubali anatumia Fomu Na. 11 na kama anakataa anatumia Fomu Na. 10 lakini TFF walikiuka yote haya.” Ameeleza Dkt. Mukangara Aidha, Dkt Mukangara ameiagiza TFF kufanya uchaguzi wa Viongozi kwa mujibu wa Katiba ya mwaka 2006 kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za BMT na kama kuna umuhimu wa kurekebisha Katiba waitishe mkutano Mkuu kwa kufuata misingi ya Katiba yao ya mwaka 2006 na kanuni za BMT kwa ajili ya kufanya maboresho hayo. Akizungumzia taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari kuwa FIFA watakuja nchini kufuatilia mgogoro wa TFF, Waziri amemwagiza Msajili wa Vyama vya michezo pamoja na TFF kuwataarifu FIFA kuhusu maelekezo yake ya kutumia Katiba ya mwaka 2006 na wawaeleze hali halisi iliyojitokeza. Amesema kuwa hakuna chama chochote cha michezo nchini kilicho juu ya BMT, hivyo vyama vyote na vilabu vyote vya michezo viendelee na shughuli zao za kuendeleza michezo kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za BMT pamoja na Katiba zao. Kumekuwepo na mgogoro katika mchakato mzima wa uchaguzi wa Viongozi wa TFF ikiwemo baadhi ya wagombea kulalamika kuenguliwa na wadau mbalimbali kulalamika kuwa haki haikutendeka na wengine kuonyesha wazi kutofuatwa kwa utaratibu wa kurekebisha Katiba hali iliyopelekea Wizara yenye dhamana ya michezo kwa kushirikiana na BMT kuingilia kati hasa katika suala la ukiukwaji wa marekebisho ya Katiba.

Thursday, 21 February 2013

Drogba wingu jeusi ligi ya mabingwa ulaya

Didier Drogba ameingia matatani, kwa madai ya kuchezea Galatasaray katika Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) bila ruhusa. Klabu ya Schalke 04 ya Ujerumani iliyotoka sare ya bao 1-1 na Galatasaray Jumatano hii, imefungua rasmi malalamiko yake dhidi ya mchezaji huyo wa Ivory Coast. Drogba alijiunga Galatasaray akitokea Shanghai Shenhua alikocheza kwa muda mfupi na kutokea utata wa mkataba na malipo yake. Shenhua pia ililalamika FIFA kwa maelezo kwamba Drogba ameondoka kinyume na mkataba unaomfunga nao bado, lakini FIFA ilitupilia mbali na kumwidhibisha kuchezea Galatasaray ya Uturuki. Katika mechi hiyo ya Ligi ya UCL ambayo Galatasaray walikuwa wenyeji, Drogba alicheza kwa dakika 90. “Kuna shaka juu ya uhalali wa kibali cha kumchezesha Drogba kwneye Ligi ya Mabingwa, Schalke 04 wana haki katika hili na wanalishughulikia,” klabu hiyo ya Ujerumani imenukuliwa ikisema. Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) limekiri kupokea malalamiko kutoka Schalke 04 juu ya uhalali wa mchezaji huyo kukipiga kwenye ligi yao. Shirikisho hilo linasema kwamba kamati yake ya nidhamu itakaa na kuchunguza suala hilo, lakini bado tarehe ya kikao haijapangwa. Drogba alijiunga Galatasaray kwenye dirisha dogo la usajili Januari mwaka huu, baada ya kukataliwa kuhama kabla ya hapo, alipoona mambo hayaendi sawa China, alikokuwa amejiunga na mwenzake, Nicolas Anelka ambaye pia ameondoka. Drobga amesaini mkataba wa miezi 18 na Galatasaray, wakati Shenhua alikuwa amesaini makubaliano ya kucheza kwa miaka miwili unusu, na alitia saini Juni mwaka jana. Ameshacheza mechi mbili Uturuki, moja ikiwa ni ya ligi Ijumaa iliyopita, alipoingia uwanjani akitokea benchi na kufunga bao dakika chache tu baada ya kuingia. Drogba aliondoka Chelsea kwa sherehe ya kutwaa ubingwa wa Ulaya na klabu hiyo ya Uingereza, ambapo mkwaju wake wa penati uliokuwa wa mwisho, ndio uliowapa rasmi Chelsea taji. Majuzi ametoka nchini Afrika Kusini, alikokuwa na timu ya taifa ya Ivory Coast – Tembo, lakini hawakufanya vizuri walivyotarajiwa, kwani waliishia robo fainali, walikotolewa na mabingwa wapya, Nigeria.